Wakimbizi kutoka CAR wahaha kujikimu nchi jirani:WFP yahitaji fedha zaidi

25 Februari 2014

Zaidi ya wakimbizi 150,000 kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati waliosaka hifadhi nchi jirani sasa wanahaha kujikimu maisha yao angalau wakidhi mahitaji ya msingi. Hali hiyo inakuja wakati shirika la mpango wa chakula duniani WFP likisema kwa kipindi cha miezi sita ijayo litahitaji karibu dola Milioni 25 kupatia msaada wa chakula wakimbizi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati walio nchi jirani. Taarifa ya Alice Kariuki inafafanua zaidi.

 (Ripoti ya Alice)

Taarifa hizo ni kwa mujibu wa WFP likisema kuwa wakimbizi hao wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wanahitaji zaidi chakula hususan chenye virutibisho lakini nchi walizokimbilia nazo hazina uhakika wa chakula.

 Nchi hizo ni pamoja na Chad yenye wakimbizi 70,000, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo 62,000 na Cameroon 28,000.

WFP inasema haiwezi kukidhi mahitaji yao kutokana na uhaba wa fedha ikisema kuwa nchi hizo ambamo wakimbizi wamekimbilia tayari zinahifadhi wakimbizi kutoka nchi nyingine. Elizabeth Byrs ni msemaji wa WFP, Geneva;

 (Sauti ya Byrs)

 “Kwa sasa hatuna fedha kusaidia wakimbizi kwenye nchi hizo. Tunaendelea kuimarisha operesheni zetu ndani ya Jamhuri ya Afrika yaKati. Hadi sasa malori 58 ya WFP yenye tani 1600 za chakula cha msaada yamewasili Bangui. Tunaendelea kutoa usaidizi huko Bassangoa, Bouar, Paoua na kwenye vijiji vingine na miji. Mwezi huu huko Bouar tulipatia chakula watu 13,000 na kwenye uwanja wa ndege Bangui sasa tunapati mgao watu 62,000.”

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter