Ban asisitiza suluhu bila ghasia nchini Ukraine

24 Februari 2014

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amerejelea wito wake wa kupatia suluhu bila ghasia mzozo unaoendelea huko Ukraine huku akisema anaendelea na mawasiliano ya karibu na wahusika wakuu jinsi ya kusaidia utatuzi wa amani wa mzozo huo.

Taarifa ya leo imemkariri Bwana Ban akisema juu ya yote anataka mchakato jumuishi wa kisiasa unaoakisi matakwa ya raia wote wa nchi hiyo huku ukihifadhi umoja wao na taifa lao.

Hata hivyo amesema ili kufanikisha hilo kwahitajika pande zote husika kujizatiti na kuazimia kufanya hiyo kwa kuzingatia misingi ya demokrasia na haki za binadamu na hivyo kuweka mazingira bora ya uchaguzi huru na wa haki.

Na katika kuonyesha mshikamano wa Umoja wa Mataifa na jumuiya kimataifa kwa ujumla na wananchi wa Ukraine, Bwana Ban amemtuma mshauri wake mwandamizi Robert Serry kwenda nchini humo huku akisema anataraji jamii ya kimataifa kutoa ushirikiano kusaidia Ukraine katika kipindi hiki kigumu.

Katika mkutano wake na Spika wa bunge Oleksander Turchinov huko Kiev, Bwana Serry amewasilisha ujumbe wa mshikamano kutoka kwa Bwana Ban na kusaidia mchakato shirikishi wa utawala.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter