Azimio la Baraza la usalama lapigia chepuo usaidizi wa kibinadamu Syria:

22 Februari 2014

Ni sauti ya Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa mwezi huu wa Februari Balozi Raimonda Murmokaite kutoka Lithuania akitangaza kupitishwa kwa kauli moja kwa azimio la baraza hilo la kuchagizi usaidizi wa kibinadamu nchini Syria ikiwemo kuwezesha watoa huduma hizo kufikia walengwa.

Azimio hilo pamoja na mambo mengine linatambua madhila yanayokumba wananchi wa Syria ambao takribani miaka mitatu sasa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yamesababisha vifo vya watu zaidi ya Laki Moja na maelfu kuwa wakimbizi ndani au nje ya nchi yao.

Halikadhalika linataka mipaka kuwa huru ili misaada kuweza kupitishwa haraka kwa walengwa huku wajumbe kupitia baraza hilo wakiazimia kuchukua hatua zaidi iwapo pande husika hazitatekeleza azimio hilo.

Punde baada ya kuptishwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akapongeza hatua hiyo huku akiweka bayana lisingalikuwa la muhimu kwani suala la usaidizi wa kibinadamu halina mjadala bali linatekelezwa kwa mujibu wa sharia za kibinadamu za kimataifa.

(Sauti ya Ban)

Katibu Mkuu akaenda mbali zaidi na kuzitaka pande kinzani ambazo ni serikali na wapinzani kuchukua hatua kusitisha machungu ya Wasyria kwani sasa yatosha na kitendo cha kuwatumia wananchi kama silaha ya vita hakikubaliki.

(Sauti ya Ban)

Naye mratibu mkuu wa masuala ya usaidizi wa kibinadamu kwenye Umoja wa Mataifa Bi.Valerie Amos amesema mzozo huo sasa na ukome kwani umeleta machungu mengi na wananchi wanataka kujenga maisha yao.