Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunategemea uongozi wako kwenye mabadiliko ya tabianchi; Ban amweleza Bloomberg

Tunategemea uongozi wako kwenye mabadiliko ya tabianchi; Ban amweleza Bloomberg

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon leo amekutana na Michael Bloomberg ambaye ni mjumbe wake maalum kuhusu miji na mabadiliko ya tabianchi na kusema ni matumaini yake kuwa Meya huyo mstaafu wa jiji la New York atatumia uzoefu wake kusaidia miji kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Akizungumza baada ya tukio maalum la kupiga picha rasmi pamoja kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Ban amesema jiji hilo lilikumbwa na zahma ya kimbunga Sandy na sasa wameweka mifumo ya kupunguza athari za majanga ya aina hiyo pindi yanapotokea.

Mathalani amesema wakati akiwa Meya, New York ilianzisha mfumo wa matumizi sahihi ya ardhi kama njia mojawapo ya kushughulikia mabadiliko ya tabianchi.

(Sauti ya Ban)

Nina uhakika tutaweza kunufaika sana na uzoefu wake, mtazamo wake wa kimataifa na uongozi na tunategemea sana uongozi wake. Tunahitaji watu wa aina yako wanaojitolea na wenye maono ya uongozi pindi tunapohaha kushughulikia suala la mabadiliko ya tabianchi.

Bwana Ban amerejelea mkutano wa kilele wa mabadiliko ya tabianchi mwezi Septemba mwaka huu akisema anamtegemea sana Bwana Bloomberg aonyeshe uongozi wake ili dunia iwe na makubaliano ya ajenda kuhusu suala hilo ifikakapo mwakani.