Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yahitaji zaidi ya dola Bilioni Mbili kunusuru mamilioni ya watoto

UNICEF yahitaji zaidi ya dola Bilioni Mbili kunusuru mamilioni ya watoto

Shirika la Umoja la kuhudumia watoto, UNICEF limetoa ombi la zaidi ya dola Bilioni Mbili kwa ajili ya usaidizi kwa watoto wenye mahitaji ya dharura kwenye nchi 50 duniani kwa mwaka huu wa 2014. Taarifa zaidi na Alice Kariuki.

(Taarifa ya Alice)

UNICEF inasema idadi hiyo ya watoto ni miongoni mwa watu Milioni 85 kwenye nchi hizo wanaohitaji misaada ya kuokoa maisha yao kutokana na mizozo, majanga ya asili na dharura nyingine za kupindukia.

Mkurugenzi wa Idara ya dharura ya UNICEF Ted Chaiban ametolea mfano Sudan Kusini ambako alizuru hivi karibuni na kushuhudia maisha ya mamilio ya watoto wasio na hatia yakiwa yamesambaratika.

Amesema msimu wa mvua unaanza na hali itakuwa mbaya zaidi. Chaiban amesema watoto hao wa Sudan Kusini ni sehemu tu ya watoto wengine wanaokumbwa na madhila kama vile Jamhuri ya Afrika ya Kati, Syria ilihali maeneo kama vile Myanmar, Colombia na Jamhuri ya Afrika ya Kati yanasahaulika kutokana na mizozo mingine inayoibuka.

(Sauti ya Ted)

Ombi hilo la UNICEF liitwalo Hatua za usaidizi wa kibinadamu kwa mwaka 2014 limeweka bayana changamoto za kibinadamu wanazopata watoto katika maisha ya kila siku ili waweze kuishi, ikiwemo ukosefu wa chanjo, elimu, ulinzi na stadi za kuwawezesha kujenga maisha yao ya baadaye.

Fedha zitakazopatikana kwenye ombi la sasa zitaimarisha usaidizi ulioanza kutolewa mwaka jana ambapo watoto Milioni 24 nukta Tano walipatiwa chanjo dhidi ya Surua na Milioni Mbili nukta Saba walipatiwa elimu.