Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya wakimbizi 20,000 wa CAR waingia Cameroon ndani ya wiki tatu

Zaidi ya wakimbizi 20,000 wa CAR waingia Cameroon ndani ya wiki tatu

Wakati Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ametoa mapendekezo sita ya kuimarisha ulinzi na usalama huko Jamhuri ya AFriak ya Kati ikiwemo kuongeza askari na polisi wa Elfu Tatu, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesema idadi ya wananchi waliokimbia makwao na kuingia Cameroon wiki tatu zilizopita ni zaidi ya Elfu Ishirini. Grace Kaneiya na Ripoti kamili.

(Taarifa ya Grace)

Idadi hiyo imetajwa kuongezeka ghafla mwezi huu kutokana na ghasia zinazoimarika kila uchao huko Jamhuri ya Afrika ya Kati. Ghasia hizo zinaongozwa na wapiganaji wa zamani wa kikundi cha Seleka na wale wanamgambo wa Anti-balaka kwenye mji mkuu Bangui na miji mingine Kaskazini magharibi mwa nchi.

UNHCR inasema idadi hii mpya inafanya wakimbizi wa CAR walioingia nchini humo baada ya waasi wa Seleka kutwaa madaraka na kukiuka haki za binadamu mwaka 2013 iwe ni zaidi ya Elfu Thelathini na Watano.

Dan McNorton ni msemaji wa UNHCR mjini Geneva;

(Sauti ya Dan)

“Jumatatu tulianza kusajili wakimbizi wapya huko Garoua Boulay na wenzetu wako Yokadouma kuthibitisha waingiao. Aidha ongezeko la wakimbizi wapya linaenda pamoja na ya chakula na mengineyo muhimu. Wenyeji wanapata athari pia kwani gharama ya kodi inapanda. Tumeanza kuhamisha wakimbizi kutoka Garoua Boulay kwenda makazi mapya ya Mborguene, ambayo yanaweza kuhifadhi watu 10,000.WAkati huo huo tunaangalia eneo lingine huko Lolo kilometa 46 kutoka mpakani ambalo linaweza kuhifadhi wakimbizi hadi Elfu Kumi na watano.”

Kabla ya janga la sasa, Cameroon tayari ilikuwa inahifadhi wakimbizi 92,000 kutoka CAR walioanza kuingia nchini humo mwaka 2006 wakikimbia vikundi vya waasi na waporaji kaskazini mwa nchi yao.