Ban asikitishwa na ghasia zilizosababisha vifo vya watu 100 huko Ukraine

20 Februari 2014

Nasikitishwa sana na kuendelea kuzorota kwa amani nchini Ukraine hususan Jumatano na Alhamisi kulikosababisha vifo vya watu 100, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon alipozungumza na waandishi wa habari mjini New York siku ya Alhamisi.

Bwana Ban amesema fikra zake ziko na familia za wafiwa huku akiwatakia ahueni ya haraka majeruhi ambapo amesema alipozungumza na Rais wa Ukraine wiki zaidi ya wiki moja iliyopita kando mwa mashindano ya Olimpiki, alimhakikishia hali inaimarika.

Amesema hilo halijatokea badala yake hali inazidi kuwa mbaya na kusababisha vifo vya watu wa pande zote za mzozo huo. Katibu mkuu ameendelea na wito wake thabiti wa kutaka kusitishwa kwa vurugu na serikali ya Ukraine ijizuie kutumia nguvu kupita kiasi kwani anachukizwa na matumizi ya silaha za moto yanayofanywa na serikali na hata waandamanaji.

Bwana Ban amesema anawasiliana na wawakilishi wa kimataiaf na amekuwa akiwasihi wote kusaidia wananchi wa Ukraine kutatua mzozo huo kwa amani kupitia mashauriano.

Amesema Umoja wa Mataifa kwa upande wake unaendelea kuwa pamoja na wananchi wote wa Ukraine na itafanya jitihada zake kusaidia suluhu la amani kwenye mzozo huo.

Katibu Mkuu alikuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kulihutubia Baraza la Usalama kuhusu mapendekezo yake ya kuimarisha hali ya usalama nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter