Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban atoa mapendekezo Sita ya kuimarisha usalama huko CAR

Ban atoa mapendekezo Sita ya kuimarisha usalama huko CAR

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon leo amelihutubia Baraza la usalama na kutoa mapendekezo Sita ya kuimarisha amani na ulinzi nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati ambako hali ya usalama inazidi kuzorota kila siku huku serikali ya mpito ikijitahidi licha ya ukata kukwamua hali ya kiusalama na kijamii.

Bwana Ban amesema pamoja na uwepo wa askari wa Muungano wa Afrika, MISCA na Ufaransa bado changamoto ni kubwa ya usalama kwani hawezi kuwepo maeneo yote na hivyo wananchi ili kuokoa maisha yao wanakimbia makazi yao na kukumbwa na madhila ya mateso na hata kuuawa.

Mapendekezo hayo ni pamoja na kuimarishwa kwa vikosi vilivyopo hivi sasa kwa kupatiwa vifaa pamoja na kuongezwa kwa askari na polisi 3000, vikosi vyote vya kimataifa huko CAR viwe na mratibu mmoja ili kuimarisha utendaji, na tatu askari wanaoongezwa wapatiwe vifaa vya kisasa akisema gharama kwa miezi sita ni dola Bilioni 38.

Halikadhalika ametaka usaidizi wa fedha kwa serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati katika kuimarisha taasisi za usalama na mahakama. Mapendekezo mengine ni..

(Sauti ya Ban)

“Tano,natoa wito kwa kuharakishwa kwa mchakato wa kisiasa na kuzuia kuendelea kwa mapingano ya kijamii na kuweka msingi wa kumaliza mzozo. Viongozi wa jamii na kidini watakuwa na dhima muhimu kwenye hilli la kuendeleza kuvumiliana, kuishi pamoja na kumaliza ghasia. Sita natoa ombi la usaidizi wa kibinadamu ambao kwa sasa umepelea katika kushughulikia janga hili. Ni asilimia 15 tu ya rasilimali zinazohitajika kwa mwaka huu zimepatikana, licha ya ahadi zilizotolewa mwezi uliopita kwenye mkutano wa Brussels.”

Katibu mkuu ameliomba baraza la Usalama kuridhia mapendekezo yake huku akitoa shukrani kwa nchi ambazo tayari zimeanza kusaidia uimarishaji wa taasisi za serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati ikiwemo Denmark iliyotoa dola Milioni Mbili na Norway ambayo imeahidi kusaidia mpango huo.

Wakati huo huo Katibu Mkuu ametangaza kuwa mwenyekiti wa Tume ya uchunguzi aliyepatiwa mamlaka na Baraza la Usalama kuchunguza ukiukwaji wa haki za binadamu huko CAR atawasili nchini humo na kundi tangulizi kuanza kaziyao.