Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sudan weka wazi ripoti ya maandamano ya mwaka jana: Mtaalamu UM

Sudan weka wazi ripoti ya maandamano ya mwaka jana: Mtaalamu UM

Mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu nchini Sudan Mashood Adebayo Baderin amehitimisha ziara yake rasmi ya siku Tisa nchini humo akitaka mamlaka kuweka hadharani ripoti ya uchunguzi ya maandamano ya Septemba mwaka jana yaliyosababisha umwagaji damu.

Bwana Baderin ameonyesha wasiwasi wake kwa serikali kutotoa ripoti ya maandamano hayo ya kupinga kuondolewa kwa ruzuku kwenye mafuta ya petroli ambapo pamoja na vifo na majeruhi, watu waliwekwa rumande, wengine kukamatwa na uharibifu wamali.

Amesema miezi mitano baada ya tukio hilo kamati iliyoundwa na serikali kuchunguza haijatoa ripoti wakati huu ambapo jamii ya kimataifa inatarajia uchunguzi wa kina wa ukiukwaji wa haki za binadamu uliotokea wakati wa maandamano hayo.

Wakati wa ziara hiyo iliyomalizika leo, Mtaalamu huru huyo alikuwa na mazungumzo na viongozi wa seriklai kuhusu hali ya haki za binadamu nchini humo pamoja na changamoto alizoibua kwenye ripoti yake ya hivi karibuni ambako bado kuna masuala yanamtia wasiwasi.

Mambo hayo ni pamoja na changamoto za haki za binadamu na pendekezo alilotoa la kutaka ushirikiano kati ya serikali ya Sudan na taasisi za kimataifa kurekebisha hali hiyo. Hata hivyo amesema wakati wa mazungumzo serikali imeonyesha nia ya kuchukua hatua huku wale wa vyama vya siasa wakitaka uwazi zaidi na demokrasia jumuishi.

Ameonya pia suala la migogoro ya kikabila na mzozo kati ya vikosi vya serikali na vikundi vilivyojihami na kutaka pande husika zimalize tofauti zao.

Bwana Baderin anatarajiwa kuwasilisha ripoti ya ziara hiyo kwenye Baraza la haki za binadamu mwezi Septemba mwaka huu.