Jamii ya kimataifa iunge mkono UM katika kuimarisha utawala wa sheria

19 Februari 2014

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amelihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakati wa kuanza kwa mjadala kuhusu uendelezaji na uimarishaji wa utawala wa kisheria na amani ya usalama duniani akitaka jamii ya kimataifa kusaidia juhudi hizo. Taarifa zaidi na Flora Nducha.

(Taarifa ya Flora)

Mjadala huo unazingatia ripoti ya Katibu Mkuu kwa Baraza la Usalama kuhusu  utawala wa kisheria wakati na baada ya mizozo ikisema usaidizi wa Umoja wa Mataifa kwenye nyanja hiyo umekuwa na manufaa kwani kule ulikopelekwa umeepusha ukwepaji wa sheria.

Akizungumza kwenye ufunguzi wa mjadala huo Bwana Ban amesema Umoja wa Mataifa unatoa usaidizi wa kuandaa Katiba, kutunga sheria na kuweka mamlaka za usimamizi wa sheria na ameteua UNDP na ofisi ya operesheni za ulinzi wa amani ndiyo waratibu wa kimataifa, lakini jitihada zake pekee hazitoshi, hivyo akatoa ombi..

(Sauti ya Ban)

“Nahamasisha wajumbe wa baraza na nchi nyingine wanachama na mashirika ya kikanda kuunga mkono  waratibu wa kimataifa na kushirikiana na Umoja wa Mataifa kuhakikisha uendelezaji wa kudumu wa taasisi za kitaifa za utawala wa sheria.”

Bwana Ban akaweka bayana hatua za kuimarisha ofisi za Umoja  huo kwenye nchi husika..

(Sauti ya Ban)

Ofisi zinapaswa kuakisi changamoto mahsusi za nchi husika na kuainisha maeneo ya kipaumbele ya usaidizi, na hili litawezesha ufanisi na uchukuaji stahili wa hatua za kisheria kwa misingi ya jinsia na pia inasaidia kutoa mwongozo na msingi wa mashauriano na mamlaka za kitaifa.”

Ripoti hiyo mathalani inataja mafanikio kuwa ni pamoja na huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambako serikali kwa ushirikiano na Umoja wa Mataifa waliweka mfumo wa kuepusha ukwepaji sheria kwa wahusika wa uhalifu wa kivita kwa kuanzisha mahakama zinazohamisha utendaji wake kutoka sehemu moja hadi nyingine ili kufikia watu wengi.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter