Pillay awaonya viongozi CAR

19 Februari 2014

Huku hali ya mashafuko ikiendelea kuangamiza maisha ya raia wasio na hatia katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa

Navi Pillay  amewakumbusha viongozi walioko kwenye vyombo vya mamlaka kuwa wanawajibu wa kisheria na akawaambia kwamba iko siku watawajibika kutokana na uhalifu wa kibinadamu unaoendelea. Taarifa zaidi na George Njogopa.

(Taarifa ya George)

Pillay amesema kuwa pamoja na kwamba ripoti kuonyesha kuwepo kwa hali ya utulivu kiasi katika mji mkuu wa Bangui lakini ukweli wa mambo ni kwamba mamia ya watu wameendelea kupoteza maisha.

Amesema tukio la hivi karibuni la kuuliwa kwa mbunge mmoja aliyetoa wito wa kuwawajibisha wale wote waliohusika na vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu  ni tukio siyo tu kwamba linaogopesha lakini linakwaza juhudi za kuanzisha mfumo unazingatia sheria na usawa.

Alilaumu baadhi ya makundi yanayoendelea kuwaandama raia wasiokuwa na hatia huki akilinyoshea kidole kundi la wanamgambo wa anti-Baraka ambalo linashutumiwa kuwa kutekeleza vitendo vya ukatili.

Aliwakumbusha viongozi waliopewa mamlaka kuchunga nyenendo zao akisema kuwa kuna siku matendo na matamshi yao yatapimwa katika mzani wa wa haki.