Pillay ataka kuepukwa matumizi ya nguvu zaidi kwenye mzozo wa Ukraini

19 Februari 2014

Huku hali ya ghasia ikiendelea kuchacha nchini Ukraine, Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Navi Pillay, amezitaka pande zilizojitumbukiza katika machafuko kujiepusha na matumizi makubwa ya nguvu.

Kauli hiyo imekuja katika wakati ambapo ripoti zikisema kuwa zaidi ya jumla ya watu 22 wamepoteza maisha wakati kulipozuka mapigano baina ya waandamanaji na polisi mjiniKievsiku ya jumanne.

Pillay amesema kuwa pande zinazohusika kwenye mzozo huo zinapaswa kujiepusha na matumizi ya nguvu yanayoweza kusababisha watu kupoteza maisha na akonya kwamba bila kuchukuliwa hatua za maridhiano hali inaweza kuwa mbaya zaidi. Cecile Pouilly ni msemaji wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa,Geneva:

(Sauti ya Cecile)

 “Tunatoa wito kwa  uchunguzi wa dharura na huru kubaini ukweli wa mambo ikiwa ni pamoja na uwezekano wa matumizi ya nguvu kupita kiasi  kwa upande wa mamlaka.  Ni muhimu kabisa kuhakikisha uwajibikaji kwa mapigano hayo hatari, la si hivyo tutaendelea kuona lawama kutoka kwa upande mmoja hadi mwingine. Kama watashindwa kufikia makubaliano wasiwasi ni kuwa tutaona ongezeko la mapigano na vurugu.”

Hapo siku ya jumanne hali ya usalama ilizorota zaidi baada ya kutokeza machafuko makubwa yaliyohusisha makundi ya watu waliandamana hadi kwenye majengo ya Bunge.