Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viongozi waandamizi wa UM ziarani CAR, IOM yatoa matokeo ya tathmini kwa wakimbizi wa ndani

Viongozi waandamizi wa UM ziarani CAR, IOM yatoa matokeo ya tathmini kwa wakimbizi wa ndani

Mratibu Mkuu wa masuala ya usaidizi wa kibinadamu kwenye Umoja wa Mataifa Bi. Valerie Amos ameanza ziara ya mbili nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati akiwa ameambana na viongozi wengine akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS, Michel Sidibe na Kamishna wa masuala ya siasa ndani ya Muungano wa AFrika Dkt. Aicha L. Abdullahi.

Habari zinasema wakiwa nchini humo watatembelea kambi za wakimbizi wa ndani na kukutana na wahanga wa janga linaloendelea nchini humo na kuwa na mazungumzo na viongozi wa kidini na wa serikali.

Zaidi ya watu 700,000 wamekimbia makazi yao nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati kutokana na mapigano yanayoelezwa kuwa ni ya kidini licha ya kuundwa kwa serikali nyingine ya mpito hivi karibuni.

Wakati huo huo shirika la kimataifa la uhamiaji, IOM limefanya awamu ya pili ya kukusanya maoni ya wakimbizi wa ndani kwenye mji mkuu Bangui ili kuona iwapo bado wana hofu ya kurejea nyumbani kama ilivyodhihirika kwenye utafiti uliotangulia mwezi mmoja uliopita.

Utafiti huo umeonyesha kuwa bado wakimbizi hao wa ndani wana hofu ya kurejea makwao kutokana na ukosefu wa usalama. Hali hiyo kwa mujibu wa IOM imesababisha watu kuishi kwenye kambi za muda nyakati za usiku na kwenda makazini nyakati za asubuhi.