Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pillay ataka hatua ya dharura ichukuliwe kufuatia ripoti kuhusu DPRK

Pillay ataka hatua ya dharura ichukuliwe kufuatia ripoti kuhusu DPRK

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa, Navi Pillay, ameikaribisha ripoti ilotolewa Jumatatu na tume huru kuhusu haki za binadamu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea, DPRK, na kusema kuwa matokeo yake yanatakiwa kuchukuliwa kama jambo la dharura.

Bi Pillay ameongeza kuwa matokeo ya uchunguzi huo yanaonyesha kuwa uhalifu dhidi ya ubinadamu unaendelea kutendeka katika DPRK kwa kiwango kilichokithiri.

Kamishna huyo mkuu amesema mnamo Januari mwaka 2013, alitoa wito kwa jamii ya kimataifa kuweka juhudi zaidi katika kukabiliana na hali ya haki za binadamu katika DPRK, tume ya uchunguzi kuundwa miezi miwili baadaye na Baraza la Haki za Binadamu.

Amesema sasa tume hiyo imechapisha ripoti ya kihistoria, ambayo inamulika uhalifu wa kiwango cha kutisha, na ambao ukubwa wake, kwa mujibu wa ripoti hiyo, hauwezi kulinganishwa na mwingine wowote ule katika dunia ya sasa. Bi Pillay ameongeza kuwa sasa hapawezi tena kuwepo kisingizio chochote cha kutochukuwa hatua.

Ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kutumia mbinu zote za kisheria kuchukua hatua, ikiwemo kuyapeleka madai ya uhalifu huo kwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC.