Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza kuu lajadili maji, usafi na nishati endelevu

Baraza kuu lajadili maji, usafi na nishati endelevu

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limefanya kikao leo kujadili kuhusu maji, usafi na nishati endelevu katika ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015. Joshua Mmali amekuwa akifuatilia kikao cha leo

TAARIFA YA JOSHUA MMALI

Rais wa Baraza Kuu, John William Ashe ameliambia baraza hilo kuwa matatizo ya maji, usafi, nishati endelevu ndiyo changamoto kuu katika duniani sasa.

“Hatuwezi tena kutofanya chochote au kukaa kimya, wakati ukosefu wa huduma za maji, kujisafi na nishati endelevu unaendelea kuwa janga la kila siku linaloyaathiri maisha ya mamilioni ya watu maskini, hususan wanawake na wasichana. Kukabiliana na matatizo haya, ni suala la lazima kimaadili kwa jamii ya kimataifa”

Katibu Mkuu Ban Ki-Moon ambaye pia amehudhuria kikao cha leo, amesema wakati kazi ya kubuni ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015, upatikanaji wa maji, usafi na nishati endelevu litakuwa suala la kipaumbele

“Jamii maskini zaidi kote duniani, mamia ya mamilioni ya watu, hususan wanawake na watoto, hupoteza muda mrefu kila siku wakitafuta kuni na maji. Madhara ya kiafya kutokana na maji chafu na uchafu wa hewa nyumbani ni makubwa. Ukosefu wa huduma za kujisafi unahatarisha zaidi afya, utu na maendeleo.”