UNHCR yapata hofu juu ya mustakbali wa wasaka hifadhi huko Manus, Papua New Guinea

18 Februari 2014

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesema lina hofu kubwa juu ya kile kinachoendelea kwenye kisiwa cha Manus huko Papua New Guinea, eneo ambako wamehamishiwa baadhi ya watu waliokuwa wanasaka hifadhi nchini Australia. Taarifa zaidi na Alice Kariuki.

(Taarifa ya Alice)

UNHCR inasema hofu hiyo inatokana na taarifa ya kwamba msaka hifadhi moja amefariki dunia na wengine kadhaa wamejeruhiwa kwenye kisiwa hicho cha Manus wakati huu ambapo inaendelea na mashauriano na serikali ya Australia huku ikikaribisha ahadi yake ya kuchunguza matukio yaliyosababisha kifo hicho.

Shirika hilo limezingatia ziara zake tatu mwaka jane kwenye kisiwa hicho kilicho Papua New Guinea na kusema limekuwa likionyesha hofu juu ya mazingira ya kuhamishia watu eneo hilo na kutokuwepo kwa ulinzi wa kutosha kwa wasaka hifadhi, wakimbizi na watu wasio na utaifa. Halikadhalika limesema ukosefu wa mfumo wa kisheria wa kupokea na kusajili wasaka hifadhi kutoka Australia bado unakabiliwa na changamoto na kuwaweka kundi hilo kwenye madhila ya kisaikolojia na kijamii. Babar Baloch ni msemaji wa UNHCR, Geneva.

(Sauti ya Babar)

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter