Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNAIDS yataka Uganda kutupilia mbali sheria dhidi ya mashoga

UNAIDS yataka Uganda kutupilia mbali sheria dhidi ya mashoga

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloongoza harakati dhidi ya Ukimwi, UNAIDS nalo limepaza sauti dhidi ya muswada wa sheria wa kupinga mapenzi ya jinsia moja nchini Uganda likisema ukiwa sheria utasababisha ongezeko la maambukizi ya virusi vya Ukimwi na kinyume na haki za binadamu.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS, Michel Sidibé amesema Uganda ilikuwa nchi ya kwanza ya kiafrika kuvunja mipaka na kujumuisha makundi ya pembezoni katika kukabiliana na ukimwi lakini sheria hiyo sasa itatumbukiza kapuni mafanikio yote yaliyopatikana.

Ametaka serikali ya Uganda kutupilia mbali muswada huo akieleza kuwa utawakuwa na madhara kwenye afya ya kijamii kwani utafiti umeonyesha kuwa mashoga wanapobaguliwa, wanakuwa na hofu kusaka huduma za kinga au tiba dhidi ya Ukimwi.

Tafiti zinaonyesha uwezekano wa mashoga kupata ukimwi kuwa ni mara 13 zaidi kuliko jamii nyingine na hivyo UNAIDS inatata huduma zitolewe bila ubaguzi wowote.