Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kenya yatakiwa kufuta vipengele vya sheria ya kuhusu umiliki wa mali kwa wanandoa

Kenya yatakiwa kufuta vipengele vya sheria ya kuhusu umiliki wa mali kwa wanandoa

Jopo la wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa leo wameisihi Kenya kufuta baadhi ya vipengele kwenye sheria ya umiliki wa mali za ndoa kwa misingi ya kwamba ni ya kibaguzi kwani inawanyima wanawake haki ya umiliki wa mali hizo iwapo kuna talaka au kifo cha mwanandoa.

Wakizungumza mjini Geneva wataalamu hao wamesema baadhi ya vipengele hivyo vipya vinataka mwanamke iwapo mume wake anafariki dunia au anampatia talaka athibitishe pasipo shaka ya kwamba alichangia kwenye upatikanaji wa mali zilizochumwa wakati wa ndoa.

Kiongozi wa jopo hilo la kikundi kazi cha Umoja wa Mataifa kuhusu sheria na kanuni baguzi dhidi ya wanawake, Frances Raday amesema kwa sheria hiyo ilivyo sasa ni wanawake wachache sana ambao wanaweza kuthibitisha suala hilo kwa kuwa ni wanawake wachache sana nchini Kenya wana hati za kumiliki ardhi zilizo na majina yao na ni wachache sana wenye hati za pamoja na waume zao.

Bi Raday amesema vipengele vya aina hiyo ni kinyume na hatua zilizopigwa kuhakikisha wananwake wanamiliki ardhi na mali na vinakiuka wajibu wa Kenya kwa utekelezaji wa haki za binadamu.

Sheria hiyo iliyoanza kutumika tarehe 16 mwezi Januari mwaka huu inaweza kusababisha wanawake wengi Kenya kushindwa kumiliki ardhi ambamo kwayo wanalima au wanaishi.

Tayari wataalamu hao huru wamefaya mashauriano na serikali ya Kenya na kuelezea utayari wao wa kusaidia kuangalia upya sheria hiyo kwa misingi ya viwango vya kimataifa vya haki za binadamu.