Mazungumzo ya Syria yamalizika bila maendeleo yoyote, Brahmi aomba radhi wasyria

15 Februari 2014

Awamu ya pili ya mazungumzo ya amani kuhusu Syria iliyokuwa inafanyika huko Geneva, Uswisi imemalizika bila maendeleo yoyote huku msuluhishi mkuu Lakhdar Brahimi akiomba radhi wananchi wa Syria kwa kitendo hicho.

Mazungumzo hayo yaliyofanyika kwa wiki mbili yalikutanisha pande zinazohasimiana nchini Syria ikiwemo serikali na upinzani ambapo Brahimi amesema pande hizo zimeshindwa kukubaliana juu ya mwendelezo wake na sasa yamehitimishwa bila kufahamu majaliwa yake.

Akizungumza na waandishi wa habari hii leo Brahimi ambaye ni Mjumbe maalum wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa nchi za kiarabu amesema ameeleza pande hizo mbili kutafakari iwapo zinataka mchakato wa amani au la…

(Sauti ya Brahimi)

 “Samahani sana na naomba radhi wananchi wa Syria kwani walikuwa na matumaini makubwa ya matokeo ya hapa. Nafikiri kile kidogo kilichotokea Homs kiliwapa matumaini kuwa ni mwanzo wa kuondokana na janga linalowasibu. Nawaomba radhi kwani katika awamu hizi mbili hatujaweza kuwasaidia. Natumai pande hizo mbili zitatathimini na kutafakari na hatimaye kuwa tayari kuzungumza kwa umakini kutekeleza makubaliano ya Geneva.”

Brahimi amesema serikali na upinzani zimekubaliana kuhusu ajenda ya awamu ya tatu kujumuisha kumaliza ghasia na ugaidi,kuundwa kwa chombo cha kitaifa cha mpito na kuanzishwa kwa taasisi za kitaifa na zile za maridhiano,ambapo kila ajenda itakuwa na siku yake lakini pande hizo bado zinatofautiana kuhusu namna ya kusonga mbele…

“Kwa bahati mbaya serikali imekataa, jambo linaloibua tashwishwi upande wa upinzani ya kwamba serikali haitaki kujadili ajenda ya chombo cha mpito. Kwa hiyo nafikiri ni vyema kila upande urejee nyumbani na kutafakuru juu ya wajibu wake. Nami vivyo hivyo nitakwenda kuzungumza na Katibu Mkuu,na pia wadau wetu wa utatu. Pia nitawapatia muhtasari wajumbe watano wa kudumu wa baraza la usalama na baraza lenyewe.”

Hakuna tarehe iliyopangwa ya kuanza kwa mazungumzo hayo ya awamu ya tatu wakati huu ambapo mzozo wa Syria uliodumu kwa miaka mitatu umesababisha vifo vya watu zaidi ya Laki Moja na maelfu kukimbilia nchi za jirani au kuwa wakimbizi wa ndani.