Ripoti mpya yaangazia madhila na mafanikio ya wahamiaji vijana duniani

14 Februari 2014

Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa imezinduliwa leo ikiangazia athari za wahamiaji vijana kwa nchi wanazotoka, kule wanakopita na hata maeneo wanakohitimishia safari zao.

Ikiwa imechapishwa na Idara ya masuala ya uchumi na kijamii ya Umoja wa Mataifa, DESA, ikiwa na jina Ripoti ya vijana duniani inabainisha mafanikio na hata madhila ya kundi hilo. Mathalani inasema kuwa vijana wanapohama nchi zao wanapata kipato kinachoboresha maisha yao, familia zao walikotoka kwa kutuma fedha lakini nchi wanamoishi ndizo zinanufaika zaidi.

Hata hivyo nchi wanakotoka zinapata madhara zaidi kwa kupoteza nguvukazi hususan kwenye sekta ya afya na elimu, imebainisha ripoti hiyo.

Ripoti hiyo inasema kutambua mazingira hayo kunatoa fursa kwa watunga sera kuelea athari za uhamiaji kwa maendeleo ya binadamu hususan vijana wa kike na wa kiume pamoja na nchi wanazotoka na wanazoenda.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo hivi sasa kuna wahamiaji Milioni 232 duniani kote ikiwa ni asilimia 3.2 ya idadi yote ya watu Bilioni 7.2 duniani. Kati yao hao Milioni 35 wana umri wa chini ya miaka 20.