CAR yamulikwa katika mjadala wa Baraza la Usalama kuhusu ushirikiano wa UM na miungano ya kikanda

14 Februari 2014

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo limefanya kikao cha kujadili ushirikiano kati ya Umoja wa Mataifa na miungano ya kikanda katika kudumisha amani na usalama wa kiamataifa- kikao ambao pia kimehutubiwa na Katibu Mkuu, Ban Ki-Moon. Joshua Mmali na taarifa kamili

(Taarifa ya Joshua)

Katika hotuba yake kwa Baraza la Usalama, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amesema kuwa ushirikiano wa Umoja wa Mataifa na miungano ya kikanda katika kudumisha amani na usalama ni sehemu ya aya ya nane ya Mkataba Mkuu wa Umoja huo, na kwamba hakuna nchi moja pekee au shirika linaloweza kukabiliana na changamoto za kuzuia mizozo, upatanishi, kukabiliana na hali za dharura, ulinzi wa amani na kujenga imani bila ushirikiano.

Bwana Ban amesifu mchango wa miungano ya kikanda, hususan Muungano wa nchi za Ulaya, EU, Muungano wa Nchi za Afrika, AU na ule wa kiuchumi wa nchi za Afrika ya Kati

“Ndiyo maana tumeimarisha ushirikiano na miungano ya kikanda, ili kuwezesha kuitikia haraka matatizo ya dharura na kuruhusu uwepo endelevu. Mada ya mjadala wa leo imekuja kwa wakati mzuri mno. Umoja wa Mataifa na wadau wake wa kikanda wanakabiliwa na mtihani mkubwa. Wingu la mauaji ya halaiki limetanda kwenye Jamhuri ya Afrika ya Kati.”