Kusuasua kutatua migogoro kwazorotesha mifumo ya usaidizi wa kibinadamu: Ripoti

14 Februari 2014

Umoja wa Mataifa kupitia shirika lake la usaidizi wa kibinadamu, OCHA, leo umezindua ripoti inayoainisha takwimu na mwelekeo wa majanga ya kibinadamu duniani ambapo pamoja na mambo mengine inasema kuwa mwaka 2012 jumla ya dola Bilioni Tano na nusu zilielekezwa kwenye usaidizi huo ikiwa ni asilimia 62 ya ombi lililotolewa.

Ripoti hiyo inasema kuwa wahisani walitoa karibu dola 18 mwaka huo ulioshuhudia majanga yakiathiri watu Milioni 124 huku zaidi ya 9500 wakiuawa. Akiwasilisha ripoti hiyo Naibu Mkuu wa OCHA Bi. Kyung-Wha Kang amesema inatoa fursa kwa makundi mbali mbali ikiwemo watunga sera, watafiti na wasaidizi wa kibinadamu kuandaa mipango yao kwani pamoja na kueleza hali ilivyokuwa inataja chanzo cha majanga na vichocheo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ongezeko la mahitaji ya kibinadamu, ukosefu wa uwezo wa kutatua majanga yanayojirudia na changamoto mpya za dunia kama vile ongezeko la idadi ya watu vimeweka mkwamo kwa serikali na hata mifumo ya usaidizi kuchukua hatua.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud