Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Redio ndicho chombo bora cha kukabiliana na ukatili wa kingono katika vita vijijini: Bangura

Redio ndicho chombo bora cha kukabiliana na ukatili wa kingono katika vita vijijini: Bangura

Leo ni siku ya Radio duniani ambapo Umoja wa Mataifa kupitia viongozi wake umechagiza ujumbe muhimu wa siku hii ambao ni usawa wa jinsia kupitia Radio kwa kuongeza watendaji wanawake na hata kuandaa vipindi vya kuimarisha usawa wa kijinsia. Assumpta Massoi na ripoti kamili.

(Taarifa ya Assumpta)

 

Miongoni mwa viongozi hao ni Katibu Mkuu Ban Ki-Moon ambaye amesema Radio ina uthabiti mkubwa wa kuweza kuvunja fikra potofu zinazoendeleza kukandamiza wanawake na watoto wa kike sehemu nyingi duniani. Zainab Hawa Bangua ambaye ni Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu kuhusu ukatili wa kingono katika maeneo ya vita, kuna umuhimu wa kila mmoja kuhakikisha kuwa wanawake jasiri ambao wanamulika hali ya maisha ya wanawake wanaodhulumiwa wanalindwa.

Amesema njia mojawapo ya kuwawezesha wanawake ni kuwapasha habari kuhusu masuala wanayopaswa kujua.

Amesema katika kazi yake, wengi waonaathiriwa na uhalifu wa ukatili wa kingono wanaishi vijijini, ambako hawana umeme na njia nzuri za usafiri, na njia pekee ya kuwafikia ni kupitia kwa redio.

“Redio, siyo tu inawaelimisha, lakini inaongeza uelewa wao, inawapa fursa zao, inawaunganisha na huduma na kuwafanya wajue kuwa kile ambacho kimekuwa kikifanyika ni uhalifu, na pia inatoa habari kwa watu wanaotenda uhalifu huo- kuwaeleza kuwa huu ni uhalifu dhidi ya sheria ya kimataifa. Kwa mfano katika DRC, hakuna mitandao ya barabara kati ya Kinshasa na Goma, kwa hiyo njia pekee ya kuwasiliana na watu hawa ni kupitia redio ya FM. Kwa hiyo nadhani redio ndicho chombo bora kabisa ambacho kimesaidia katika kukabiliana na tatizo la ukatili wa kingono”