Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ripoti kuhusu idadi ya watu na maendeleo yazinduliwa

Ripoti kuhusu idadi ya watu na maendeleo yazinduliwa

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon leo ameshiriki uzinduzi wa ripoti tathmini ya idadi ya watu na maendeleo kwa mwaka huu wa 2014. Taarifa kamili na Asumpta Massoi.

(Tarifa ya Asumpta)

Ripoti hiyo ya kamati ya kutathmini utekelezaji wa mpango uliopitishwa mwaka 1994 kwenye mkutano wa kimataifa wa idadi ya watu huko Cairo, ICPD imeonyesha mafanikio ya huduma za afya ya uzazi ambayo ni msingi kwa maendeleo ya mtu binafsi, familia, taifa na dunia kwa ujumla, amesema Bwana Ban wakati akirejelea takwimu za ripoti hiyo, huku akitanabaisha kuwa bado kuna changamoto kubwa zinazokwamisha baadhi ya maeneo kufikia viwango vinavyotakiwa kwa mujibu wa malengo ya maendeleo ya milenia hivyo akasema….

(Bwana Ban)

"Hebu turejelee ujumbe mkuu wa ICPD na tujizatiti kwenye dira ya CAIRO ya mustakhabli bora wa wote unaotaka kuendeleza afya ya watu wote, kujenga uwezo wa watu na kuzingatia utu wa kila mtu na haki za binadamu kila mahali.”

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Idadi ya watu duniani, UNFPA Babatunde Osotemehin akasema kuwa ripoti hiyo ni ushuhuda wa mafanikio ya miaka 20 iliyopita akitolea mfano wa kile walichoshuhudia..

(Babatunde)

"Idadi vifo vya wajawazito wakijifungua imepungua kwa karibu asilimia 50 duniani kote kati ya mwaka 1990 hadi 2010. Wanaweke wengi zaidi leo wana fursa ya kwenda shule, ajira na hata kushiriki siasa. Watoto wengi hususan wa kike wanaendesha shule ambapo uandikishaji shule ya msingi unakaribia asilimia 90.”

Kwa mujibu wa ripoti hiyo takribani watu bilioni Moja wameondokana na ufukara wa kupindukia katika miongo miwili iliyopita lakini bado kuna tofauti kubwa ya kipato kitaifa na hata kimataifa huku masuala ya ndoa za umri mdogo na ubakaji yakitajwa kuwa miongoni mwa vikwazo vya maendeleo ya watu hususan wanawake na watoto wa kike.