Hifadhi ya chakula CAR ni mbaya:FAO

12 Februari 2014

Wakulima katika Jamhuri ya Afrika ya Kati wanahitaji msaada wa haraka wa mbegu kwa ajili ya kufanikisha shughuli za kilimo zinazoaanza mwezi Machi,hatua ambayo inaweza kupunguza kwa kiwango kikubwa tatizo la njaa na utapiamlo ambao imekuwa ikiandaa taifa hilo. Hii ni kwa mujibu wa shirika la chakula na kilimo FAO

 (Taarifa ya George)

Hifadhi ya chakula katika taifa hilo inaripotiwa kuwa ya kiwango cha chini kutokana na mavuno hafifu yaliyopatikana msimu uliopita wa mwaka 2013.

Machafuko ya wenyewe kwa wenyewe ambayo yamesababisha maelfu ya raia kwenda mtawanyikoni yalivurugu kwa kiwango kikubwa shughuli za kilimo.

Kulingana na mwakilishi wa FAO nchini humo Alexis Bonte anasema kuwa kufanikisha msimu wa kilimo unaoanza mwezi ujao, ndiyo utakaoweza kulifanya taifa hilo kurejea kwenye hali salama ya chakula.

Inakadiriwa kwamba zaidi ya asilimia 75 ya raia nchini humo wanategemea shughuli ndogo ndogo za kilimo kwa ajili ya kujipatia kipato.

Kwa upande wake Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa zaidi ya watu milioni 2.5 katika Jamhuri hiyo wanahitaji misaada ya dharura kwa ajili ya kujikwamua na hali ngumu wanayokumbana nayo.