Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mshikamano wa dunia ni muhimu kudhibiti utoroshaji wa fedha kutoka Afrika

Mshikamano wa dunia ni muhimu kudhibiti utoroshaji wa fedha kutoka Afrika

Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki amesisitiza umuhimu wa mshikamano wa kimataifa katika kuhakikisha suala la utoroshaji wa fedha kutoka Afrika linatokomezwa.

Mbeki ambaye ni mwenyekiti mwenza wa jopo la Tume ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika na Muungano wa Afrika amesema hayo alipozungumza na waandishi wa habari mjini New York, Marekani.

Amesema hivi karibuni walitembelea nchi kadhaa za Afrika kujionea halisi mathalani vile ambavyo utoroshaji fedha unavyoathiri nchi hizo.

"Jopo linaangalia suala hilo hususan utoroshaji unafanyika vipi kwa kuwa mwishoni tunapaswa kusema hatua zipi zinahitajika kuzuia. Kwa sababu ni vyema kueleza inatokeaje, zinatoroshwaje barani Afrika lakini pia kuelezea zinaishia wapi. Na ni dhahiri kuwa nchi zinazopokea fedha hizo ni zile zilizoendelea na zile zenye misamaha ya kodi.”

Takribani dola Bilioni 50 hupotea barani Afrika kila mwaka kwa kutoroshwa nje ya bara hilo, na hivyo kuzidi hata kiwango cha misaada rasmi ya maendeleo bara hilo hupokea.