Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ghasia CAR zasababisha maelfu kukimbilia Cameroon

Ghasia CAR zasababisha maelfu kukimbilia Cameroon

Maelfu ya raia wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR wamekimbilia Cameroon katika siku chache zilizopita kutokana na mapigano kati ya vikundi vya waasi vinavyopingana na hiyo ni kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR kama anavyoripoti Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Katika siku Kumi zilizopita watu 9,000 wamewasili Kentzou, mashariki mwa Cameroon na wengi wao ni raia wa CAR, pamoja na Cameroon, Nigeria na Mali.

Takwimu hiyo zinafanya idadi ya wakimbizi wa CAR huko Cameroon kufikia 20,000.

Simulizi zao ni mapigano makali kati ya wanamgambo wa Seleka na wale waopinga kile cha Balaka kwenye mji mkuu Bangui na mingineyo kaskazini magharibi mwa nchi. Fatoumata Lejeune-Kaba ni msemaji wa UNHCR huko Geneva, Uswisi.

(Sauti ya Fatoumata Lejeune-Kaba)

 “Wengi wao ni waislamu wanaodai kuwa wana hofu ya usalama kwa sababu wanaonekana kuonea huruma kundi la Seleka. Mazingira ya maisha ni magumu kwa wengi waliosaka hifadhi kwenye familia, misikitini, mitaani au uwanja wa michezo. UNHCR inafanya kazi kubadili eneo la jirani lililotengwa na serikali ili wakimbizi hao wahamishiwe ifikapo mwishoni mwa wiki.”

Zaidi ya raia 838,000 wamepoteza makazi CAR na nusu yao wanaishi kambi za muda mjini Bangui ambako  yaelezwa kuna uwezekano mkubwa wa mlipuko wa kipindupindu kutokana na msongamano wa watu na uksoefu wa maji safi na huduma za kujisafi.