Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kusuasua kwa ratiba ya kuharibu mpango wa kemikali Syria kwatia wasiwasi:

Kusuasua kwa ratiba ya kuharibu mpango wa kemikali Syria kwatia wasiwasi:

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo wamesikiliza ripoti ya maendeleo ya kazi ya kuharibu mpango wa silaha za kemikali wa Syria ambapo wameonyesha wasiwasi wake juu ya kusuasua kwa utekelezaji wa ratiba husika.

Ripoti hiyo iliwasilishwa na Mratibu wa jopo la pamoja la Umoja wa Mataifa na shirika la kimataifa la kupinga silaha za kemikali, OPCW Bi. Sigrid Kaag katika mashauriano ya faragha.

Rais wa Baraza hilo kwa mwezi huu wa Februari Balozi Raimonda Murmokaitė kutoka Lithuania amewaambia waandishi wa habari kuwa wajumbe wametambua kuondolewa kwa kiwango kidogo tu cha kemikali kutoka Syria kupitia bandari ya Lattakia tareheSabana 27 Januari mwaka huu.

Wamesema wanatambua kuwa Syria ina uwezo wa kuchagiza mpango huo kwa hiyo imeitaka ihakikishe unazingaria ratiba ya kuhitimishwa tarehe 30 Juni mwaka huu.

“Wamesisitiza kuwa ni wajibu wa serikali ya Syra kuhakikisha kuondolewa na kuteketeza mpango wake wa silaha za kemikali kwa muda unaotakiwa na mazingira salama. Wamekaribisha hatua zilizochukuliwa na jopo la pamoja za kuimarisha usalama wake na taratibu za ulinzi wakati huu wa mazingira hatarishi na yasiyotabirika na kuendelea kwa vitisho dhidi ya wajumbe wa jopo hilo.”

Naye Bi. Kaag amesema vikwazo vya kuondosha kemikali hatarishi zaidi nje ya nchi vinakabilika na kwamba watahakikisha tarehe inazingatiwa wakati huu ambapo hata uteketezaji wa kemikali ndani ya nchi unaendelea.