Ban asifu uwezo wa michezo kuleta watu pamoja

6 Februari 2014

Huku ikiwa imesalia siku moja kabla ya kuanza mashindano ya Olimpiki ya Msimu wa baridi huko Sochi, Urusi, Katibu Mkuu Ban Ki-Moon amesema michezo ina uwezo wa kuwaleta watu pamoja, kwani inavuka mipaka yote, huku akitoa wito wa amani ya Olimpiki kwa wote wanaozozana. Joshua Mmali na taarifa kamili

Taarifa ya Joshua

Bwana Ban amesema Umoja wa Mataifa na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki, IOC, hazishindani katika michuano hiyo ya Olimpiki, bali zinaungana katika ndoto za pamoja za uendelevu, utangamano, mshikamano, kutobaguana, na usawa wa watu wote.

Amesema mashindano ya Olimpiki yanaonyesha uwezo wa michezo kuleta watu pamoja, bila kujali umri wao, rangi, tabaka, dini, ulemavu, jinsia, mienendo yao kimapenzi au jinsia wanazojitabulisha nazo.

Amesema makundi mengi yanakutana kwenye uwanja wa michezo, na sio uwanja au kitali cha vita.

“Katika kazi yangu, mie huhudhuria hafla nyingi zinazozileta nchi pamoja kwa masuala ya vita, umaskini, majanga na matatizo mengine. Leo nipo Sochi kushuhudia nchi zikija pamoja katika moyo wa mashindano ya kirafiki na heri njema. Narejelea wito wangu kwa wote walio vitani kuweka chini silaha zao wakati wa Olimpiki, na kuangazia ahadi ya amani. Kama Katibu Mkuu, natoa wito kwa pande zote zinazozozana kuheshimu amani ya Olimpiki, hususan nchini Syria, Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati.”