Nchi tatu za Afrika zapongezwa kwa kuchukua hatua dhidi ya Ukeketeaji wanawake

6 Februari 2014

Wakati leo ni siku ya kimataifa ya kutokomeza ukeketaji kwa watoto wa kike na wanawake, Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa watu, UNFPA limetoa heko kwa Uganda, Kenya na Guinea-Bissau kwa kutunga sheria zinazoharamisha ukeketaji.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA Babatunde Osotimehin katika ujumbe wake wa siku ya leo amesema hayo ni mafanikio wakati ambapoEthiopiailichukua hatua dhidi ya ngariba na wazazi wa watoto Sita wa kike.

Amesema hatua hizo ni za kuigwa kwani ukeketaji haukubaliki kwa kuwa unakiuka haki za binadamu na kuendelea kutishia maisha na majaliwa ya watoto wa kike na wanawake wengi.

Bwana Osotimehin amesema kwa kufanyiwa vitendo hivyo afya zao zinakuwa mashakani, halikadhalika ustawi wa familia zao, jamii na taifa kwa ujumla.

Mkuu huyo wa UNFPA amesema changamoto za kuondokana na mila hiyo potofu zinakabilika na hivyo ushirikiano wa pande zote utachagiza kuleta mabadiliko chanya na hakikisho la ustawi wa wanawake na watoto wa kike duniani.

Barani Afrika na Mashariki ya Kati, UNFPA inakadiria kuwa wanawake na wasichana Milioni 125 wamekeketwa