Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kamati kuhusu haki za mtoto yaitaka Holy See kutoficha uhalifu dhidi ya watoto

Kamati kuhusu haki za mtoto yaitaka Holy See kutoficha uhalifu dhidi ya watoto

Kamati ya kimataifa kuhusu haki za watoto imeelezea kusikitishwa na hatua za kuwahamisha mapadri wanaotenda ukatili wa kingono dhidi ya watoto kutoka parokia moja hadi nyingine au kutoka nchi moja hadi nyingine ili kujaribu kuvificha vitendo hivyo ambavyo vimeripotiwa na tume kadhaa za kitaifa za uchunguzi. Hayo yameibuka huko Geneva, Uswisi wakati kamati hiyo ikihitimisha tathmini ya haki za watoto katika Holy See, ambayo ni mamlaka ya inayowakilisha Vatican au kanisa Katoliki. Assumpta Massoi na taarifa kamili

Taarifa Assumpta Massoi

Kamati hiyo imesema kuwa kutokana na sheria inayowabana wana-kanisa kutosema chochote kwa kuhofia kufukuzwa kanisani, visa vya uhalifu wa kingono dhidi ya watoto havijakuwa vikiripotiwa kwa mamlaka za sheria katika nchi ambako uhalifu huo unatendwa.

Badala yake, visa vya watawa na mapadri kutelekezwa, kushushwa madaraka au kufutwa kazi kwa sababu hawakutii sheria ya kutosema chochote vimeripotiwa kwa kamati hiyo kuhusu haki za watoto.

Halikadhalika, vimeripotiwa visa vya mapadri wengine kupongezwa kwa kukataa kuwakemea watu wanaotenda uhalifu wa kingono dhidi ya watoto, kama kile kilichoshuhudiwa katika waraka ulotumwa na Kadinali Castillon Hojos kwa Kasisi Pierre Pican mnamo mwaka 2001. Kirsten Sandberg ni mwenyekitio wa kamati hiyo

(Sauti ya Kirsten)

“Kwanza idadi ya matukio ambayo walitoa ushirikiano na mamlaka za kitaifa hatufahamu, hawajafichua takwimu zozote kutoka kwenye kumbukumbu zao, lini walitoa ushirikiano, visa vingapi wanafahamu, hatujui chochote kuhusu takwimu hizo, ambazo Holy See wanaweza kuwa nazo. Visa vingi ni vya zamani na waathirika ni watu wazima sasa.Na kuna visa vya watoto kunyanyaswa na bado ni watoto, na hatufahamu ni visa vingapi bado vinaendelea.”

Kamati hiyo imetoa wito kwa Holy See kufanyia marekebisho sheria ya kanisa ili ukatili wa kingono dhidi ya watoto uchukuliwe kama uhalifu na sio tu kama vitendo vinavyokiuka maadili, pamoja na kuondoa sheria zote zinazowalazimu waathiriwa na mashahidi wa uhalifu huo kubaki kimya.