Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto Syria wanakabiliwa na madhila yasiyoelezeka:UM

Watoto Syria wanakabiliwa na madhila yasiyoelezeka:UM

Watoto nchini Syria wamekuwa wakikabiliwa na madhila yasiyoelezeka kwa karibu miaka mitatu sasa ya vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo imesema ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu jinsi vita vinavyoathiri vijana.

Ripoti hiyo inaishutumu serikali ya Syria na washirika wake ambao ni wanamgambo kwa kuhusuka na mauaji yasiyohesabika pamoja na ukatili na utesaji wa watoto.

Pia ripoti imewalaumu wapinzani nchini humo kwa kuingiza vijana wadogo vitani na kutumia mbinu za kigaidi katika maeneo ya raia. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ametoa wito wa kumaliza machafuko.

Ripoti hiyo inajumuisha kipindi cha kuanzia Machi 2011 hadi Novemba mwaka jana ,vita ambavyo hadi sasa vimeshakatili maisha ya watu zaidi ya 100,000.

Wiki iliyopita wawakilishi wa serikali na upande wa upinzani  walikutana kwa ajili ya mazungumzo ya amani mjini Geneva , lakini hawakuweza kupata njia ya kumaliza machafuko nchini mwao.