Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtu mwingine afariki Saudia kutokana na kuambukizwa homa ya Corona

Mtu mwingine afariki Saudia kutokana na kuambukizwa homa ya Corona

Shirika la Afya Duniani, WHO, limesema kuwa mnamo Januari 28, Wizara ya Afya nchini Saudi Arabia ilitangaza kuwa mtu mmoja zaidi amethibitishwa kuambukizwa homa ya kirusi cha corona (MERS-CoV) kufuatia vipimo vya maabara.

Mtu huyo ni mwanamume mwenye umri wa miaka 60 kutoka Riyadh, ambaye alianza kuumwa mnamo Januari 19, akiwa na dalili za homa hiyo. Alilazwa hospitalini mnamo tarehe 24, na kufariki mnamo Januari 28. Sampuli za maabara zilichukuliwa na  kupelekwa kwenye maabara kuu ya Riyadh, na kuthibitisha kuwa ilikuwa homa ya MERS-CoV. Mtu huyo anasemekana kuwahi kukaribiana na mtu aliyethibitishwa kuwa na homa ya kirusi cha corona.

WHO pia imeelezewa na Muungano wa Kiarabu wa Emirates (UAE) kuwa mwanamume muuguzi kutoka Dubai mwenye umri wa miaka 33 aliiaga dunia mnamo Januari 16 kutokana na homa hiyo.

Tangu Septemba 2012, WHO imefahamishwa kuhusu jumla ya visa 181 vilivyothibitishwa katika maabara vya homa ya corona, vikiwemo vifo 79.