Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuwa kisiwa hakuepushi Seychelles dhidi ya usafirishaji haramu wa binadamu: Mtaalamu UM

Kuwa kisiwa hakuepushi Seychelles dhidi ya usafirishaji haramu wa binadamu: Mtaalamu UM

Ni jambo lisilo na mjadala kuwa Seychelles ni kisiwa lakini hakiko salama dhidi ya wasafirishaji haramu wa binadamu na vitendo vingine viovu.

Hiyo ni kauli ya Joy Ngozi Ezeilo mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa dhidi ya usafirishaji haramu wa binadamu, kauli aliyotoa baada ya kuhitimisha ziara yake nchini Seychelles.

Amesema hilo liko bayana kwani usafirishaji haramu wa binadamu ni jambo lilnalofanyika kisiri nchini humo na limeweza kuendelea kutokana na watu kutokuwa na taarifa sahihi, jambo linalosababisha ukosefu wa takwimu.

Bi. Ezeilo amesema kisiwa hicho chenye idadi ndogo ya watu kinapata ugeni mkubwa wa watalii na hata wahamiaji wafanyakazi jambo linalodokeza kuwepo kwa usafirishaji haramu hususan kwa watoto wa kike kutoka Ulaya Mashariki wanaotumbukizwa kwenye Utalii wa ngono.

Hata hivyo amesema utashi wa kisiasa wa mamlaka za Seychelles uko dhahiri na ametambua kitendo cha serikali kuridhia mikataba ya kimataifa na hata kuunda kamati ya kitaifa ya kudhibiti usafirishaji haramu wa binadamu.

Amesema hatua hizo zitakuwa na uthabiti iwapo kutakuwepo na muundo wa kisheria na kisera .

Ripoti kamili ya Bi. Ezeilo ataiwasilisha wakati wa kikao cha Baraza la Haki za binadamu mwezi Juni mwaka huu huko Geneva.