Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kasi zaidi yahitajika kuondosha kemikali za sumu Syria: OPCW

Kasi zaidi yahitajika kuondosha kemikali za sumu Syria: OPCW

Baraza tendaji la shirika la kimataifa la kupinga matumizi ya silaha za kemikali, OPCW limepokea taarifa kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Ahmet Üzümcü kuhusu jitihada zinazoendelea za kuharakisha kazi ya kuondoa kemikali za sumu nchini Syria.

Kemikali hizo ni zile ambazo zinatakiwa kuthbitishwa na kuteketezwa nje ya nchi hiyo ambapo Bwana Üzümcü amesema shehena mbili zimeondolewa mwezi huu ikiashiria mwanzo wa kazi hiyo lakini suala la kuongeza kasi zaidi liko bayana.

Amesema mbinu zozote zapaswa kusakwa ili kuweka mwendelezo wa mchakato huo ili kutoa hakikisho kwa nchi zinazosaidia kazi hiyo kwamba kazi inaendelea na si imetelekezwa.

Bwana Üzümcü amewaeleza kuwa amezungumza na maafisa waandamizi wa Syria ambapo amewajulisha umuhimu wa kuzingatia muda wa utekelezaji wa kazi hiyo kwa mujibu wa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na taarifa ya baraza hilo.

Kazi ya kutokomeza mpango wa silaha za kemikali nchini Syria inatekelezwa na jopo la pamoja la Umoja wa Mataifa na OPCW.