Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tiba ya wote dhidi ya TB kufanyika nchini Niger

Tiba ya wote dhidi ya TB kufanyika nchini Niger

Shirikisho la kimataifa la Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu, IFRC, pamoja na Mfuko wa Kimataifa wa kukabiliana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria, Global Fund, wametia saini makubaliano ya ufadhili wa matibabu kwa wote nchini Niger dhidi ya ugonjwa wa kifua kikuu, ambayo ni moja ya nchi zenye viwango vya juu zaidi vya maambukizi ya ugonjwa huo katika ukanda wa Afrika Magharibi.

Ufadhili huo wa miaka miwili, kutoka mfuko wa Global Fund,  ambao ni wa thamani ya Euro Milioni 10, utasaidia kuwawezesha watu wote wanaokadiriwa kuwa milioni 17 nchini Niger kupimwa na kupata huduma za matibabu.

 Fedha hizo zitaongezwa ili kupeleka huduma za matibabu ya kifua kikuu kwa watu wapatao 26,000 katika vituo 200 vya matibabu ifikapo mwaka 2015, zikilenga jamii zilizomo hatarini zaidi, zikiwemo zile za wafugaji.