Manyanyaso na vitisho dhidi ya waandishi wa habari Misri hayakubaliki: Pillay

31 Januari 2014

Umoja wa Mataifa umeelezea wasiwasi wake juu ya hutuma zinazoibuliwa dhidi ya waandishi wa habari nchini Misri ya kwamba wanaunga mkono magaidi. Assumpta Massoi na ripoti kamili.

(Taarifa ya Assumpta)

Umoja huo kupitia Kamishna wake Mkuu wa Haki za Binadamu Navi Pillay umesema tuhuma hizo zinasababisha manyanyaso na vitisho dhidi ya vyombo vya habari ni kinyume na haki ya uhuru wa kujieleza na kutoa maoni nchini humo.

Bi. Pillay ametaja mashtaka ya kusaidia kikundi cha kigaidi na kutishia usalama wa kitaifa yaliyofunguliwa dhidi ya wanahabari 16 wa Misri na wengine wanne wa kigeni wanaofanyia shirika la Al Jazeera na kusema kuwa hayana msingi wowote.

Rupert Colville ni msemaji wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa.

 Hawa ni watu ambao wanabeba kamera na siyo bunduki. Kamera zinasaka kuangazia kile kinachotokea na siyo kuziba utoaji taarifa. Ni jambo la kipekee kubaini jambo hili linajumuishwa kwenye mjadala kuwa waandishi wa habari wanasaidia ugaidi. Haya ni mambo yanayotia hofu na tunatumai yatabadilika haraka. Tumepokea pia taarifa za vitisho kwa wanahabari ambao vifaa vyao vilichukuliwa na kwingineno wanahabari wa Misri kufukuzwa kazi kwa kuandika habari nyeti na wengine kuswekwa rumande. Tunaisihi serikali ya Misri kuwaachia huru ili waendelee na jukumu lao ambalo ni haki ya msingi.

Ofisi hiyo ya haki za binadamu imetaka uchunguzi huru na wa uwazi wa taarifa za ghasia dhidi ya waandishi wa habari.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter