Mazungumzo ya leo yalikuwa na mvutano na matumaini vile vile: Brahimi

30 Januari 2014

Siku ya nne ya mazungumzo kati ya pande kinzani kwenye mzozo wa Syria imehitimishwa huko Geneva, Uswisi huku msuluhishi mkuu Bwana Lakhdar Brahimi akisema kuwa siku ya leo licha ya mvutano mkubwa angalau kulikuwepo na matumaini.

Akizungumza na waandishi wa habari, Brahimi ambaye ni mjumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa nchi za kiarabu, ametolea mfano wa suala hali ya usalama na ugaidi nchini Syria ambalo alisema liibua mvutano.

Amesema kuna makubaliano kuwa ugaidi upoSyrialakini hakuna makubaliano jinsi ya kukabiliana nalo. Brahimi akataja jambo ambalo liliridhiwa kila upande..

Upande wa upinzani ulipendekeza dakika moja ya ukimya kuenzi wale wote waliouawa nchini Syria bila kujali ni wanatoka kambi gani, na ujumbe wa serikali mara moja ulikubali hoja hiyo na tulitulia kwa dakika moja.”

Alipoulizwa ripoti kuwa misaada bado haijafikaHomslicha ya makubaliano ya Jumapili, Brahimi amesema..

"Bila shaka nimevunjika moyo, nimevunjika moyo sana kwa sababu hali Homs ni mbaya na imekuwa mbaya kwa miezi kadhaa. Kwa hiyo angalau misaada imefika Yarmouk lakini hakuna suluhu kwa Homs”

Kuhusu hitimisho la awamu ya kwanza ya mazungumzo hayo iliyoanza Jumatatu, Brahimi amesema itakuwa ni kesho Ijumaa na bado hajafahamu iwapo watakuwa na azimio au tamko la hitimisho ya awamu hiyo tayari kwa awamu ya pili.