Zaidi ya watu 700,000 watawanywa na machafuko Sudan Kusini:Amos

29 Januari 2014

Mkuu wa shirika la Umoja wa mataifa la kuratibu la misaada ya kibinadamu na huduma za dharura OCHA Bi Valarie Amos amesema watu zaidi ya laki saba wametawanywa na machafuko yanayoendelea Sudan Kusini katika wiki saba zilizopita. Flora Nducha na taarifa kamili

(TAARIFA YA FLORA NDUCHA)

Bi Amos ambaye yuko ziarani Sudan Kusini amesema akiwa mjini Malakal ameshuhudia hali mbaya kukiwa na upungufu wa chakula , watu wanaishi katika mazingira duni , machafu huku kukiwa na dhiki ya maji.

Amesema watoto wengi hawako shuleni na mahitaji ya afya yanazidi kuongezeka.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Juba Bi Amos amesema wanawake wamelazimika kutembea mwendo mrefu na kwa siku kadhaa ili kupata ulinzi na msaada na kuna maelfu ya watu ambao bado wanahitaji msaada wa haraka.

(SAUTI YA VALARIE AMOS)

"Nimekutana na wananwake wengi ambao wametembea muda mrefu wakitafuta msaada na usaidizi, watoto ambao wametenganishwa na wazazi wakikimbia machafuko na watu ambao wanasema  walikuwa wanlengwa na kufanyiwa ukatili kwa sababu ya kabila lao au kwa sababu ya mwelekeo wao wa kisiasa. Kwa sasa Mashirika ya kutoa misaada yamesaidia zaidi ya watu 300,000. hata kama maisha ya wengi yameokolewa lakini hatujaweza kutoa msaada kwa wengine wengi kwa sababu ya ukosefu wa usalama"