Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban aisifu Cuba kwa mchango wake kwenye tiba, asema ni wa kuigwa

Ban aisifu Cuba kwa mchango wake kwenye tiba, asema ni wa kuigwa

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametembelea chuo kikubwa zaidi ya tiba duniani kilichoko nchini Cuba kijulikanacho kama ELAM na kushukuru nchi hiyo kwa vile ilivyo mstari wa mbele kwenye kuimarisha ushirikiano wa nchi za Kusini hasa kwenye masuala ya tiba.

Akizungumza kwenye chuo hicho amesema mchango huo wa kihistoria wa Cuba uko dhahiri kwani mara nyingi anapotembelea nchi zinazoendelea, idadi kubwa ya mawaziri wa afya au maafisa wa afya wanamueleza kuwa wamepatiwa mafunzo nchini Cuba.

Bwana Ban amesema ndani na nje ya nchi yao madaktari wa Cuba wako na wagonjwa katika shida na raha kuhakikisha wanatoa huduma hiyo kwa manufaa ambapo huwa wa kwanza kufika kwenye majanga na wa mwisho kuondoka akitolea mfano Haiti.

(Sauti ya Ban)

"ELAM imetoa mafunzo kwa makumi ya maelfu ya wanafunzi, lakini Cuba inaweza kufundisha dunia nzima kuhusu huduma ya afya. Nataka kuungana na wengine wengi kupongeza mfumo wa afya wa Cuba ulioweka mizizi yake kwenye huduma ya afya ya msingi ambayo imekuwa na matokeo ya kipekee.”

Ametaja mafanikio hayo ya kipekee kuwa ni pamoja na Idadi ndogo ya vifo vya watoto wachanga, umri wa juu wa kuishi, na huduma ya afya kwa wote, mambo ambayo amesema yanapaswa kuigwa katika dunia ya leo.