Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mazungumzo ya Geneva yasuasua lakini kuendelea Jumatano

Mazungumzo ya Geneva yasuasua lakini kuendelea Jumatano

Mwakilishi Maalum wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Nchi za Kiarabu, Lakhdar Brahimi, amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kuwa amezishauri pande zinazohusika katika mazungumzo ya amani kuhusu Syria kuahirisha kikao cha Jumanne mchana, ili zipate fursa ya kujiandaa tena na kurejelea kikao bora zaidi cha mazungumzo hayo hapo kesho Jumatano asubuhi.

Bwana Brahimi amesema mazungumzo hayo hayajakuwa rahisi, na hayatakuwa rahisi hata katika siku chache zijazo.

“Lakini nafurahi kuwa mmeambiwa na pande zote mbili kuwa zina nia ya kubaki hapa na kuendelea na mazungumzo haya hadi Ijumaa, Kwa hiyo hakuna mtu anayeondoka. Hamna anayekimbia”

Bwana Brahimi amesema upande wa upinzani umewasilisha maoni yake kuhusu jinsi ya kutekeleza mapendekezo ya mkutano wa Geneva ya Juni 30, mwaka 2012, lakini upande wa serikali bado.

“serikali haijafanya hivyo, lakini tumejadili kuhusu masuala kadhaa. Kwa hiyo mnajua , hatujafikia mafanikio yoyote, lakini bado tunajikita katika mazungumzo haya, na hilo pekee ni jambo zuri kwa mtazamo wangu.”