Huduma kwa wagonjwa walio taabani ni zaidi ya tiba: Ripoti mpya

28 Januari 2014

Mtu mmoja kati ya watu 10 ndiye anayepata huduma ya tiba ya kupunguza maumivu ya magonjwa anapokuwa taabani na kukaribia kupoteza maisha, imesema ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa Jumanne ikitaka mataifa kujumuisha huduma hiyo ya tiba kwenye mifumo yao ya afya.

Ripoti hiyo ikionyesha mahitaji ya huduma hiyo duniani kote imechapishwa kwa ushirikiano kati ya shirika la afya duniani, WHO na ushirikiano wa huduma za kupunguza machungu ya magonjwa mtu awapo taabani, WPCA.

Mathalani ripoti inaeleza kuwa theluthi moja ya watu wanaohitaji huduma hiyo ni wagonjwa wa saratani, moyo, ini, figo na Ukimwi huku ikitanabaisha kuwa huduma wanayohitaji watu hao si kupunguza maumivu pekee bali pia matatizo ya kisaikolojia na usaidizi kwa familia zinazowauguza.

Dkt. Cecilia Sepulveda ni mshauri mwandamizi wa WHO kuhusu kinga dhidi ya magonjwa sugu.

(Dkt. Sepulveda)

(Dkt. Sepulveda)

"Kwa hiyo twapaswa kuwafikia hao wagonjwa na kujaribu kupunguza machungu yao na pia kusaidia familia zao. Ripoti hii inaotoa makadirio haya lakini pia inaonyesha maeneo ya upatikanaji wa huduma. Na iwapo utaiangalia utagundua mahitaji mengi yasiyokidhiwa. Ni mtu mmoja tu kati ya 10 ambao wanapata huduma hiyo. Na idadi kubwa ya wanaohitaji wako kwenye nchi za vipato vya chini au kati ambako wanakabilliwa na mzigo mkubwa.”

 

Suala la huduma kwa wagonjwa walio taabani linatarajiwa kujadiliwa katika mkutano wa 67 wa mwaka wa WHO utakaofanyika mwezi Mei mwaka huu huko Geneva, Uswisi.