Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lajadili hali CAR na Burundi

Baraza la Usalama lajadili hali CAR na Burundi

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, limekutana leo kujadili hali nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, na pia kujadili hali nchini Burudi, likizingatia ripoti ya Katibu Mkuu kuhusu ofisi ya Umoja wa Mataifa Burundi. Joshua Mmali na taarifa kamili

(Taarifa ya Joshua)

Baraza la Usalama limeanza shughuli zake hii leo kwa kupitisha kwa kauli moja azimio la kuongeza muda wa huduma za ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, BINUCA, kwa kipindi cha mwaka mmoja hadi Januari 31 mwaka 2015. Ofisi hiyo pia itapanuliwa ili isaidie katika harakati za mpito wa kisiasa na katika juhudi za maridhiano.

Kuhusu Burundi, Baraza hilo limesikiliza ripoti ya Katibu Mkuu, ambayo imewasilishwa na Mwakilishi wake Maalum ambaye pia ni Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Burundi, BINUB

Parfait Onanga-Anyanga akisema amejawa na matumaini kuhusu taifa la Burundi, lakini bado kazi ya upatikanaji amani ya kudumu haijakamilika. Amesema Warundi wanatakiwa kuchukua jukumu la kuendeleza juhudi za kulijenga taifa lao wenyewe

Katibu Mkuu ametoa wito wa Warundi kuonyesha uongozi wa busara tunapoendelea mbele, hususan tukizingatia changamoto kubwa ambazo bado zipo. Sina shaka kuwa watafanya hivyo, na najua kwamba Baraza hili litaendelea kuwaunga mkono. Tusichoke kufanya kilicho kizuri. Lakini ni lazima tufanye hivyo, na tunaweza tu kufanya hivyo tukiungwa mkono kikamilifu na serikali ya Burundi.”