Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Licha ya mafanikio, Rwanda iweke fursa ya demokrasia ya kweli: Mtaalamu UM

Licha ya mafanikio, Rwanda iweke fursa ya demokrasia ya kweli: Mtaalamu UM

Mtaalam maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya kufanya mikutano ya amani na haki ya kujumuika, Maina Kiai, amesifu Rwanda kwa maendeleo yake ya kiuchumi miaka 20 baada ya mauaji ya kimbari huku akitaka nchi hiyo kuondoa vikwazo dhidi ya mijumuiko ya amani.

Amesema hatua hiyo itawezesha kupanua wigo wa mafanikio yake hadi kwenye nyanja za demokrasia ya vyama vingi na haki za binadamu.

Bwana Kiai amesema hayo mwishoni mwa ziara yake rasmi nchini Rwanda akisema kuwa baada ya mafanikio ya kiuchumi na  ujenzi wa taasisi za kuendeleza utulivu na usalama, hatua inayopaswa kufuatia ni ile ya kuweka misingi ya demokrasia ya kweli ya vyama vingi.

Katiba yaRwandainaruhusu uhuru wa kujumuika kwa amani lakini mtaalamu huyo amesema kimatendo kuna vikwazo vya usajili, shughuli za vikundi vya kiraia na hata serikali kuingilia masuala ya ndani ya vikundi vinavyoonekana kukosoa sera za serikali.

Ametolea mfano chama cha Green Party ambacho amesema kimefanikiwa usajili baada ya miaka minne huku vyama vingine kadhaa vya upinzani vikiwa havijasajiliwa.

Wakati wa ziara hiyo ya siku nane, Bwana Kiai alikuwa na mazungumzo na maafisa wa serikali, mahakama, wawakilishi wa vikundi vya kiraia na wanadiplomasia, na ripoti yake ataiwasilisha kwenye baraza la haki za binadmau mwei Juni mwaka huu