Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mauaji ya kimbari ya Wayahudi yakumbukwa kwenye UM

Mauaji ya kimbari ya Wayahudi yakumbukwa kwenye UM

Hafla ya kumbukumbu ya mauaji ya kimbari yalotekelezwa dhidi ya Wayahudi, yaani Holocaust, imefanyika leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa. Siku hii ni maadhimisho ya kila mwaka ya kufunguliwa kwa kambi ya mauaji ya kimbari ya Auschwitz, na kumbukumbu kwa wahanga wa mauaji hayo..

Muziki

Rais wa Baraza Kuu, John William Ashe, amesema siku hii ni wakati wa kukumbuka hofu na uchungu waloupitia wale walohamishiwa kwenye kambi za halaiki mbali na familia zao, na miaka mingi ya mateso na hali ya kudhalilisha katika kambi hizo.

“Kwa wale walonusurika, tunakumbuka mseto wa mshangao na furaha ya uhuru baada ya miaka ya kuwa mateka, vikifuatiwa na mzigo wa kuanza tena upya na makovu ya kimawazo na kimwili. Wengi hapa tunaijua safari ya Holocaust kupitia hadithi za kijasiri tunazoambiwa na manusura ambao walirudi na kutuhadithia kuhusu machungu walokumbana nayo. Hadithi zao zimetushangaza na ujasiri wao kuigusa mioyo yetu.”

Katika ujumbe wake wa video, Katibu Mkuu Ban Ki-Moon amesema siku hii ni ukumbusho wa mateso walopitia mamilioni ya watu waso na hatia, na kumulika kwa machungu yatokanayo na chuki dhidi ya uyahudi na chuki za aina nyingine yoyote ile.

 “Umoja wa Mataifa ulianzishwa ili kuzuia janga kama la Holocaust kuwahi kutokea tena, lakini majanga ya Cambodia, Rwanda na Srebrenica yalitokea tena, na hivyo kuonyesha kuwa sumu ya chuki ya mauaji ya kimbari bado inaenea. Tunapaswa kufanya kila liwezekanalo ili kukabiliana na fikra za kueneza chuki na ubaguzi.”

 Baadhi ya watu maarufu walohudhuria hafla hiyo ni mtunga filamu, Steven Spielberg na Rena Finder, mmoja wa manusura aliyekuwa kwenye orodha ya Oskar Schindler, ambaye aliwanusuru.