Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pillay aitaka Misri kujizuia na ghasia na kufanya uchunguzi

Pillay aitaka Misri kujizuia na ghasia na kufanya uchunguzi

Kamishina mkuu wa haki za binadamu  Navi Pillay Jumatatu amesema anatiwa mashaka makubwa na ghasia zinazoendelea nchini Misri katika siku za karibuni ambazo zimesababisha idadi kubwa ya vifo na majeruhi.

Ametoa wito wa kufanyika mara moja uchunguzi wa matukio yaliyosababisha vifo vya takribani watu 62 Jumamosi na wengine wengi kujeruhiwa.

Pillay amezitaka pande zote kujizuia na ghasia zaidi. Ameongeza kuwa majeshi ya usalama yanawajibu wa kuheshimu haki za waandamanaji wa amani na ni muhimu kwa uongozi wa Misri kutekeleza wajibu wake wa kimataifa na kuhakikisha Wamisri wote wanatekeleza haki zao za uhuru wa kukusanyika na kujieleza bila hofu ya ghasia au kukamatwa.

Na kwa upende wa waandamanaji Bi Pillay amewataka kuhakikisha kwamba maandamano yao yanasalia kuwa ya amani. Pillay amesisitiza kwamba wakati wote vikosi vya usalama Misri ni lazima vifanye kazi kwa kuzingatia haki za kimataifa , sheria na viwango vinavyostahili kuhusu matumizi ya nguvu.