Shehena nyingine ya vifaa vya kemikali yaondoshwa Syria

27 Januari 2014

Jopo la pamoja la Umoja wa Mataifa na shirika la kimataifa la kupinga silaha za kemikali lenye jukumu la kutokomeza mpango wa silaha za kemikali nchini Syria limetoa taarifa juu ya kuondoshwa kwa shehena nyingine yenye vifaa vinavyohusiana na mpango huo.

Taarifa hiyo inasema shehena hiyo ilipakiwa kwenye meli za mizigo kutoka Norway na Denmark kwenye bandari ya Lattakia baada ya kukaguliwa na kuthibithswana maafisa kutoka jopo hilo.

Meli hizo ziling’oa nanga na kuanza safari chini ya uangalizi wa usalama wa majini kutoka meli za China, Denmark, Norway na Urusi.

Jopo hilo limesema linatumai kuwa serikali ya Syria itaendelea na jitihada za kukamilisha uondoshaji wa vifaa vinavyohusiana na silaha za kemikali kwa njia salama na kwa kuzingatia muda uliopangwa kwa mujibu wa uamuzi wa baraza tendaji la OPCW na azimio la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.

Shehena ya kwanza ikiwa na kemikali hatari zaidi iliondoka bandari ya Lattakia tarehe Saba mwezi Januari na meli husika kutia nanga kwenye bandari ya Gioia Tauro tayari kwa vifaa husika kuhamishiwa kwenye meli ya kimarekani MV Cape Ray.