Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lajadili tishio la ugaidi na hali nchini Côte d’Ivoire

Baraza la Usalama lajadili tishio la ugaidi na hali nchini Côte d’Ivoire

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo limekutana kujadili tishio la vitendo vya kigaidi dhidi ya amani na usalama wa kimataifa, pamoja hali nchini Côte d’Ivoire. Joshua Mmali na taarifa kamili

Wanachama wa Baraza hilo wameanza majadiliano yao kwa kupitisha kwa kauli moja azimio namba 2133, la mwaka 2014, ambalo linahusu kupiga vita ugaidi na ufadhili wa vitendo vya kigaidi.

Katika azimio hilo, wamerejelea azimio namba 1373 la mwaka 2001 linalozitaka nchi zote kuzuia ufadhili wa vitendo vya kigaidi, na kujiepusha na kutoa aina yoyote ya msaada kwa watu wanaohusika na vitendo vya kigaidi. Azimio hilo pia linazitaka nchi wanachama kuhakikisha raia wao au watu walio katika ndani ya mipaka yao hawatoi misaada yoyote au ufadhili kwa watu wanaotenda vitendo vya kigaidi.

Baraza la Usalama pia limesikiliza ripoti ya Katibu Mkuu kuhusu hali nchini Côte d’Ivoire. Akilihutubia Baraza hilo, Mwakilishi wa Katibu Mkuu na Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Côte d’Ivoire, Bi Aïchatou Mindaoudou, amesema licha ya hatua nzuri zilizopigwa hadi sasa na kujizatiti kwa serikali, taifa hilo limeendelea kukabiliana na changamoto za kiusalama na hali bado ni tete

Matukio ya mara kwa mara ya ghasia za kikabila na baina ya jamii pamoja na wizi wa kutumia silaha na uhalifu wa kupangwa vimeendelea kutishia usalama na utulivu. Vyombo vya usalama vya kitaifa bado vinahitaji kufanyiwa marekebisho makubwa. Kutokuwepo msimamo dhahiri kuhusu hatma ya baadhi ya watu, kunachangia ukosefu wa usalama na kuhatarisha haki za binadamu za wananchi”