Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashauriano na pande mbili za Syria yanatia moyo: Brahimi

Mashauriano na pande mbili za Syria yanatia moyo: Brahimi

Mjumbe maalum wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Nchi za kiarabu kwenye mzozo wa Syria, Lakhdar Brahimi ameanza mazungumzo kwa nyakati tofauti na pande mbili zinazokinzana nchini humo huko Geneva, Uswisi ambapo amewaeleza waandishi wa habari kuwa mazungumzo hayo yamekuwa ya kutia moyo na yataendelea kesho.

Bwana Brahimi amesema pande zote mbili zinatambua kuwa msingi wa majadiliano yao ni tamko la pamoja la Geneva la tarehe 30 Juni 2012 na kuridhiwa na azimio la baraza la usalama namba 2118. Amesema kamwe hawajatarajia mashauriano hayo kuwa rahisi..

(Sauti ya Brahimi)

"Kamwe hatukutarajia iwe rahisi na nina uhakika haitakuwa rahisi, lakini naamini pande zote zinafahamu hali ilivyo , nchi yao iko katika hali mbaya sana. Nafikiri watu walioko hapa wakiwakilisha upinzani na serikali wanafahamu vyema kama ninavyofahamu mimi au zaidi, ni nchi yao hata hivyo.”

Bwana Brahimi alipotakiwa atoe ufafanuzi juu ya ripoti kuwa baadhi ya wajumbe wamesema wataondoka Jumamosi kurejea Syria iwapo hakuna maendeleo yoyote kwenye majadiliano hayo, Mjumbe huyo amesema..

(Sauti ya Brahimi)

"Tutakutana kesho, natumai itakuwa mwanzo mzuri na tutaendelea hadi mwishoni mwa wiki ijayo, penginepo na bila shaka kuna wakati tutaahirisha kwa siku chache li kutoa fursa ya watu kuondoka na hatimaye kurejea na kuendelea.. Tulikuja hapa tukitambua haitakuwa rahisi, haitakuwa rahisi dakika yoyote lakini tunafanya tuwezalo ili kusongesha mbele."

Mazungumzo hayo ya Geneva yanayohusisha pande tatu ambazo ni ujumbe kutoka serikali ya Syria, wawakilishi wa upinzani na Bwana Brahimi yanafuatia mazungumzo ya Montreux yaliyolenga kuonyesha mshikamano na watu wa Syria katika kutatua mzozo nchini mwao.