Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mamia ya mamilioni ya ekari za ardhi huenda zikaharibiwa ifikapo 2050: UNEP

Mamia ya mamilioni ya ekari za ardhi huenda zikaharibiwa ifikapo 2050: UNEP

Ardhi ya asili yenye ukubwa wa ekari milioni 849 kote duniani, ambayo ni karibu sawa na eleo la ardhi nzima ya taifa la Brazil, huenda ikaharibiwa ifikapo mwaka 2050, ikiwa mienendo ya sasa ya matumizi ya ardhi yasiyo endelevu itaendelea, imeonya ripoti ya Shirika la Mpango wa Mazingira katika Umoja wa Mataifa, UNEP.

Katika ripoti hiyo ilotolewa wakati wa kongamano la kimataifa kuhusu uchumi mjini Davos, Uswisi, UNEP imesema haja ya kulisha idadi kubwa ya watu inayozidi kuongezeka kote duniani imepelekea ardhi zaidi kugeuzwa mashamba ya mimea ya chakula badala ya nyasi na misitu.

Ripoti hiyo iitwayo, Tathmini ya Matumizi ya Ardhi Duniani: kusawazisha matumizi na uzalishaji endelevu, imesema hali hiyo imechangia uharibifu wa mazingira na kupotezwa kwa bayo anuai, na hivyo kuathiri asilimia 23 ya ardhi kote duniani. Achim Steiner ni Mkurugenzi Mkuu wa UNEP:

“Katika sekta ya kilimo, ardhi imefikia mahali ambapo sasa uwezo wake wa kutoa mazao umepunguwa katika uzalishaji wa kilimo ambao umekuwa ukiongezeka. Tunaharibu pia ardhi, tukipoteza rutuba, na tunakabiliwa pia na changamoto ya rasilmali ya maji. Kwa hiyo kutolewa kwa ripoti hii kuhusu ardhi kunahusu kile kinachotendeka kwa sayari yetu, na haja ya kujaribu kupanga tena chumi zetu, na kuweka mkakati wa kuchukua mkondo wa mfumo endelevu wa fedha katika uchumi unaojali mazingira.”